MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare, amefanya ziara ya Ukaguzi wa Miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa na lengo la kuboresha kasi ya uwajibikaji na upatikanaji mzuri wa huduma kwa wananchi.
Ziara hiyo imeanza leo Februari 28 , 2020 katika Kata ya Mlimani ikiwa ni moja ya ziara zake ambazo analenga kuzifanya katika Kata zote 29 zilizopo Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, RC Sanare, ameanza ziara yake katika Shule ya Msingi Benard Bendel isiyo ya Serikali iliyopo Kata ya Kichangani kufuatia maagizo aliyoyatoa katika Uongozi wa shule hiyo kuhusiana na ukarabati wa miundombinu ya Bweni la Wanafunzi wa Kiume .
Aidha, RC Sanare, baada ya ukaguzi huo wa bweni amejidhirisha kwamba maagizo aliyoyatoa yamefanyiwa kazi na sasa Bweni hilo lipo tayari kwa ajili ya matumizi kwa wanafunzi.
"Nipo hapa shuleni kwa ajili ya kuangalia nilichokiagiza, kwakweli hali haikuwa nzuri katika Bweni la wanafunzi hivyo katika kikao changu nilimuagiza Mwalimu Mkuu kuhakikisha yale mapungufu yaliyopo katika Bweni la wanafunzi wa Kiume yanafanyiwa kazi na sasa nimejiridhisha kwa macho yangu kwamba hakuna shida tena , napenda kusema sasa rasmi wanafunzi wanawezakulitumia bweni hilo lakini pale mnapoona kuna shida na mnataka msaada wa Kiserikali msisite kutuambia nasi tutawapatia ushirikiano lengo ni kuboresha elimu katika Shule zetu zilizopo katika Mkoa wetu wa Morogoro na umeniambia una shule nyingine usisite nitakuja kikubwa nenda kaweke mazingira vizuri "Amesema RC Sanare.
Pia amesema lengo la kufanya ziara katika shule binafsi ya Bernard Bendel ni kuhakikisha kwamba wana boresha miundombinu ili kuongeza viwango vya ufaulu kwani katika takwimu za viwango vya ufaulu katika ngazi za Mkoa hawaangalii shule za Serikali pekee bali waangalia matokeo kwa ujumla katika Mkoa mzima.
Pia amemuagiza Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro kusimamia majengo ya Shule kikamilifu kuanzia shule za Serikali pamoja na zile binafsi pamoja na kusisitisha ujenzi kwa kuweka alama ya X majengo yote ambayo yanajengwa bila ya vibali vya ujenzi.
Katika ukaguzi huo wa maendeleo shuleni, hakuishia katika shule hiyo pekee bali amepata nafasi ya kutembelea Shule ya Sekondari Bungodimwe iliyopo Kata ya Mlimani na kukagua Ujenzi wa vyumba viwili vya Madarasa vilivyomalizika na kugharimu shilingi Milioni 25 na laki 9.
Amesema kuwa, kwa jinsi Ujenzi huo ulivyokamilika ameridhika na ujenzi huo na kusema thamani ya pesa inaonekana huku akiwapongeza sana Wananchi kwa jitihada walizozionesha aidha amesema bado nguvu za Wananchi zinahitajika ili kuendelea kutanua miundombinu ya shule hiyo Ikiwemo ukarabati wa Madarasa, ujenzi wa Jengo la Utawala , Maabara pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Shule.
Pia amewataka TARURA , kuichonga barabara hiyo inayowaunganisha wananchi wa Towelo yenye urefu wa KM 3.5 kutoka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
"Ndugu zangu TARURA mliniambia kwamba mlishaipitisha barabara hii katika Bajeti ya Mwaka 2020/2021 lakini mpaka leo sioni utekelezaji, sijaridhishwa na majibu yenu ya kupunguza bajeti kwahiyo hao viongozi wenu wa Makao Makuu wakija naomba nikutane nao na niwalete waone kama watapunguza laa, ombi langu ni kwamba iangalieni hii barabara kwa jicho la huruma ili kunusuru watoto wetu kuacha utoro, wanafunzi kufika kwa urahisi na wananchi pia kunufaika na huduma hii muhimu" Amesisitizia RC Sanare.
Kwa upande Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, ameiomba TARURA kuwapatia njia nzuri ili magari yaweze kufikika katika Shule hiyo ili kurahisisha usafiri kwa Walimu na Wanafunzi pamoja na Wananchi wanaoitumia barabara hiyo japo sio kwa kiwango cha lami lakini hata kuchonga sehemu korofi itasaidia.
"Barabara hii ni muhimu sana , hivyo mkiitengeneza vizuri itakuwa si mkombozi wa wanafunzi pekee bali hata kwa wananchi wanoitumia barabara hii watanufaika na huduma hii ya barabara , walimu watakuja shuleni, utoro kwa wanafunzi utapungua kutokana na taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Shule hii ya Bungodimwe, na wakazi wa huku wataitumia kwa ajili ya kusafirisha bidhaa zao na kwenda pamoja na kurudi majumbani "Amesema DC Chonjo.
Aidha RC Sanare amewataka Wanafunzi wasome kwa bidii na kuacha kucheza ili waweze kutimiza ndoto zao katika maisha na kuwa Viongozi bora wa Taifa ili kubadilisha maendeleo hususani watoto wa kike kwani viongozi wengi wa kike duniani ni kwamba wameaminiwa kulingana na elimu zao.
Pia RC Sanare,ameahidi kuchangia shilingi Milioni Moja pamoja na Mkuu wa Wilaya shilingi laki 5 kwa ajili ya uboreshaji wa maendeleo katika shule hiyo.
Amesema Wazazi Katika kata hiyo ni wagumu kuchangia elimu lakini furaha yake ni kuona baada ya miaka 5 au 10 viongozi wa Morogoro wanapatikana katika Shule za Morogoro.
Katika hatua nyingine, amewataka Watendaji wa Halmshauri ya Manispaa ya Morogoro kuanzia ngazi za Mitaa na Kata wawe na utaratibu wa kusoma mapato na matumizi katika vikao vyao wanapokuatana na wananchi kwani suala hilo lipo kisheria na agenda kubwa ziwe ni kujadili ulinzi na usalama pamoja na mapato na matumizi kabla hawajaingia katika ajenda mpya.
Agizo hilo amelitoa kufuatia malalamiko ya wananchi katika kikao cha wazi kilichofanyika katika Ofisi ya Kata ya Mlimani huku baadhi ya wananchi wakilalamikia Uongozi wa Kata pamoja na Mitaa kutosoma mapato na matumizi jambo linalowapelekea kutokuwa na uelewano mzuri kati ya wananchi na viongozi wa kata hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, amempongeza Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuwapatia fedha shule zote za Manispaa ya Morogoro kupitia mpango wa Elimu bure bila malipo pamoja na pesa za miradi ya maendeleo hususani miradi ya kimkakati , Mkuu wa mkoa Morogoro Mhe. Loata Sanare kwa hatua za kuboresha maendeleo ya elimu , Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mhe. Regina Chonjo ya usimamizi mzuri wa miradi na kazi kubwa na nzuri wanazozifanya ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Aidha amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Abdulaziz Abood kufuatia kutoa pesa nyingi za mfuko wa Jimbo pamoja na pesa zake binafsi katika kuchangia maendeleo ya Manispaa ya Morogoro.
Naye Mstahiki meya wa Manispaa ya Morogoro, mhe. Pascal Kihanga, amesema shule za Manispaa ya Morogoro zinakabiliwa na changamoto nyingi hivyo amemuomba Mkuu wa Mkoa kueleza na kuwapa maelekezo pale anapoona kuna makosa ili wajirekebishe kuliko kuyaacha na kuwagharimu baadae.
Kihanga, amewataka Wazazi kuendelea kuchangia pesa na vifaa mbalimbali ili kuleta maendeleo katika shule hiyo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa