Wananchi wametakiwa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo uhaba wa vyumba vya madarasa.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa vyumba nane vya madarasa vya Shule ya Sekondari Mkundi inayojengwa na nguvu za wananchi wa Kata hiyo wakishirikiana na Serikali,Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe.Abdulaziz Abood amesema ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo na kupongeza jitihada hizo za wananchi wa Kata ya Mkundi.
Baada ya kuridhishwa na jitihada hizo za wananchi wa Mkundi,Mhe. Abood amejitolea mifuko 125 ya saruji yenye thamani ya shilingi Milioni tatu na laki mbili na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kufanikisha ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Mkundi na wananchi wa Kata hiyo wamemshukuru Mhe. Abood kwa kuwapatia msaada huo na wamesema kuwa shule hiyo kwa asilimia kubwa itasaidia kupunguza msongomano wa wanafunzi katika shule ya Sekondari Kingo ambayo inamilikiwa na Kata ya Kingo, hivyo wanafunzi wa Kata ya Mkundi kulazimika kusoma katika shule hiyo kutokana na Kata yao kukosa Shule ya Sekondari.
Msaada huo alioutoa Mheshimiwa Abood ni mwendelezo wa utekelezaji wa ahadi zake na kuunga mkono jitihada za wananchi na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo la Morogoro mjini.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa