Wanawake wameendelea kujitokeza kutoa msaada wa mahitaji ya msingi kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro, walioathiriwa na mafuriko yalitokana na mvua nyingi zilizonyesha hasa tarehe 24.01.2024.
Leo, tarehe 06.02.2024, wanawake wa kikundi cha Jiendeleze Women Association (JIWA), chenye Ofisi yake kwenye kata ya Kihonda, wamemkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, mheshimiwa Rebbeca Nsemwa kilo 175 za unga wa ugali, sabuni za miche na za unga, pamoja na nguo na viatu ikiwa ni msaada wao kwa waathirika wa mafuriko.
Mheshimiwa Nsemwa amewashukuru sana wanawake hao wajasiriamali kwa tendo lao la huruma kwa wananchi wake na ametoa wito kwa ye yote atakayeguswa kuendelea kujitokeza kutoa misaada kwa ajili ya wananchi wenzetu ambao baadhi yao nyumba zao zilibomoka, na wengine vitu vyao vyote vilisombwa na maji vikiwemo vyakula na mavazi.
“Ninyi ni kundi la pili la wanawake mliokuja kutoa msaada kwa ndugu zetu. Kundi la kwanza lilikuwa la Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT). Salamu zenu hizi nitazifisha kwa Mkuu wetu wa Mkoa pia. Binafsi nimefurahi sana kupokea kundi hili, na ninatoa wito kwa wanaume nao wajitokeze” alisema mheshimiwa Nsemwa.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Bi. Doroth Luoga amesema dhumuni la kikundi chao ni kusaidiana wao kwa wao na kusaidia jamii inayowazunguka. Baada ya kuona jinsi wananchi wenzao walivyoathiriwa na mafuriko, walikubaliana kuchangishana ili kutoa mkono huo wa pole.
Naye mratibu waMaafa wa Manispaa ya Morogoro, ndugu Elizabeth Badi amesema kwa sasa kipaumbele cha misaada hiyo ni kwa wananchi wenye hali duni kiuchumi, ambao wameathiriwa na mafuriko.
“Unajua miongoni mwa walioathiriwa na mafuriko, wapo watu ambao mafuriko ni kana kwamba yamekuja kuwaongezea ugumu wa maisha na hawana pa kushika. Hao ndio ambao kwa sasa misaada hii tunaielekeza kwao” alifafanua Badi.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa