MRATIBU wa TASAF Halmshauri ya Manispaa ya Morogoro, Feliciana Katemana, amewataka Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia TASAF kutumia fursa hiyo kwa ukamilifu kwa kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza azma ya serikali ya kupambana na umaskini nchini.
Hayo ameyasema leo Januari 16. 2020 wakati akikagua na kujionea utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii-TASAF katika Kata ya Mwembesongo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inafanya juhudi kubwa za kuweka mazingira mazuri kwa Wananchi kujiletea maendeleo na kuboresha maisha yao hivyo akawataka kutumia vizuri fursa hiyo kwa kufanya kazi za uzalishaji mali kwa bidii ili kukuza uchumi wao na hatimaye kuchangia katika pato la taifa na kuondoa kero ya umaskini miongoni mwao kwa vitendo.
Amesema kuwa Manispaa ya Morogoro katika mradi wa TASAF imepokea jumla ya Shilingi Milioni 119 ambazo zilikuwa ni za kipindi cha Mwezi Machi na Aprili kwa mwaka jana 2019 huku akiwataka Wananchi kuwa na subira kwani Serikali yao ni tulivu na itawapatia watu wote walio na sifa katika mradi huo bila ubaguzi wa aina yoyote.
Hata hivyo amesema kuwa , fedha hizo zimegawiwa kwa walengwa wapatao 2945 katika kata zote 29 za Manispaa ya Morogoro katika Mitaa 164.
Katemana amewataka Walengwa wa TASAF kutobweteka na mafanikio waliyoanza kuyapata kutokana na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia TASAF badala yake waendelee kuuchukia umaskini kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii ili hatimaye waweze kuboresha maisha yao huku akisisitiza ustawi wa jamii kwa ujumla hususani watoto kama ilivyo dhamira ya Serikali.
Katika hatua nyingine , Katemana , amewashauri maafisa maendeleo na ustawi wa jamii wanaosimamia mpango wa TASAF katika ngazi za Kata kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa na kuzingatia Uzalendo kwani amesema Mfuko huo unagusa nyanja muhimu za Maendeleo ya Wananchi katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya,maji,uchumi,kilimo,mifugo na hifadhi ya mazingira na hivyo kuwa miongoni mwa sekta zinazogusa maisha ya wananchi wengi moja kwa moja.
“Serikali inathamini mchango wa taasisi hii katika jitihada zake za kupunguza umaskini nchini, endeleeni kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa haraka na ufanisi mkubwa” amesisitiza Katemana.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo yaliyochangiwa kwa kiwango kikubwa na Serikali,Wadau wa Maendeleo na Wananchi hususani Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao amesema kwa sehemu kubwa wameanza kuboresha maisha yao na kuonyesha namna wanavyouchukia umaskini kwa vitendo.
Kwa upande wake, mnufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini , Bunga Mogela, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Magufuli huku akikiri kuwa mpango huo umekuwa mkombozi mkubwa kwao kwani umeweza kuwabadilisha kimaisha na kuiomba serikali kuongeza kiwango cha ruzuku ili kilingane na thamani halisi ya fedha kwa sasa.
Naye Antari Shadadi, mkazi wa kata ya Mwembesongo, amesema kuwa kwa sasa anajishughulisha na ununuzi wa Mkaa pamoja na kusomesha Watoto kupitia biashara hiyo huku akimuomba Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kuendelea na moyo huo huo wa kuwasaidia walala hoi na watu wenye vipato vya chini katika Kaya Masikini.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa