WASIMAMIZI wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ngazi ya Kata na Mitaa Manispaa ya Morogoro wamepatiwa mafunzo maalum yanayolenga Kutoa mwongozo wa namna ya kusimamia Shughuli za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unatarajia kufanyika Novemba 27,2024.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa ya Morogoro,Emmanuel Mkongo, katika Ukumbi wa Tanzanite Hall Septemba 30/2024.
Akizungumza na wasimamizi hao, amewakumbusha kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu zote za uchaguzi pamoja na kusisitiza umuhimu wa kutunza siri zote zinazohusu mchakato mzima wa uchaguzi.
Hata hivyo, Mkongo, ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kujiandikisha ili kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa.
“Kila mwananchi mwenye sifa ya kushiriki uchaguzi huu asisite kutumia haki yake ya kikatiba ya kupiga kura,” Ameongeza Mkongo.
Aidha,Mkongo, amewataka wakazi wenye umri wa miaka ishirini na moja au zaidi wanaotaka kugombea nafasi ya uenyekiti wa Mtaa , Ujumbe kuchukua fomu za kugombea zinazopatikana kwenye ofisi ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi.
Sambamba na hilo ,amewataka wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili wawe na uelewa wa kutosha katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya mwanzo Morogoro Mjini, Mbaraka Mchopa, amewakumbusha wasimamizi hao kuheshimu viapo vyao kwa uaminifu na kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni, na taratibu zote za uchaguzi katika utendaji wao.
Kwa upande wa Afisa Uchaguzi Manispaa ya Morogoro,Shabani Duru, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwafanya wasimaizi kuwa na uadilifu na umakini katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia uchaguzi.
Mada nyingine zilizo wasilishwa na waratibu wa uchaguzi ngazi ya Wilaya ni pamoja na matumizi ya fomu mbalimbali za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, maadili ya Utumishi wa umma kwa watumishi wanaohusika katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, upokeaji na utunzaji wa vifaa vya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, tehama,uhamasishaji wa Wananchi kushiriki shughuli zote za uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, kuhabarisha umma juu ya masuala ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na uandaaji wa Taarifa za uchaguzi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa