Tuesday 3rd, December 2024
@HALMASHAURI YA MANISPAA YA MOROGORO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU KATIKA WILAYA YA MOROGORO
Mimi Regina Reginald Chonjo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro napenda kuwaarifu kuwa kama ilivyo ada Mwenge wa Uhuru hukimbizwa kila mwaka katika Wilaya zote za Jamhuri ya muungano wa Tanzania Bara na Visiwani, katika kipindi chote umekuwa ni kichocheo cha maendeleo. Napenda kuwataarifu kuwa Mwenge wa Uhuru ambao hukimbizwa Nchi nzima tutaupokea Wilayani Morogoro tarehe 21.7.2018 ukitokea Mkoani Pwani. Tutaupokea Bwawani, mpakani mwa Mikoa ya Pwani na Morogoro.
Kwa Wilaya yetu, Mwenge wa Uhuru unategemea kuona, kuzindua na kuwekwa mawe ya Msingi katika miradi ya maendeleo katika Nyanja mbalimbali.
Ndugu wananchi wa Wilaya ya Morogoro, ninayo furaha kubwa kwa mapokezi mazuri ya Mwenge wa Uhuru mwaka jana na kuiwezesha Wilaya yetu ya Morogoro Mjini kushika nafasi ya kwanza Kimkoa mwaka 2017. Hii ilitokana na ushirikiano wa pamoja na mshikamano mliouonesha. Nawashukuru sana, naomba tushirikiane tena mwaka huu kuilinda na kuitetea nafasi yetu. Ushindi unatokana na muitikio wenu kwa wingi, uchangamfu, ukarimu na muonekano wa miradi yetu ya maendeleo ambayo sina wasiwasi na ubora wake (value for money).
Ndugu wananchi, kwa Manispaa ya Morogoro napenda kuwajulisha kuwa mkesha wa mbio za Mwenge utafanyika katika viwanja vya Kiwanja cha Ndege ambapo maonesho ya vikundi mbalimbali yatafanyika sambamba na burudani za vikundi mbalimbali vya sanaa na muziki vitakuwepo na hatimaye tunategemea kuukabidhi Wilaya ya Gairo siku ya Jumapili Asubuhi tarehe 22/07/2018.
Pia tarehe 24.7.2018, Mwenge wa Uhuru utapokelewa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ukitokea Wilaya ya Mvomero na kukimbizwa katika miradi ya Tarafa ya Mikese na kukabidhiwa Halmashauri ya Ifakara tarehe 25.7.2018.
Unawashwa ili ulete Matumaini, maendeleo, maisha mazuri, usalama, heshima, utu wa Binadamu bila ubaguzi wa Dini, kabila, wenye nacho na wasionacho.
Kauli mbiu 2018:- ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA: WEKEZA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU.
Kauli Mbiu hii inaenda sambamba na Juhudi za Mhe. Rais John Pombe Magufuli:-
Ili maendeleo haya na Juhudi hizi za Mhe. Rais ziweze kufanikiwa na kuzaa matunda zitahitaji wananchi wenye Elimu:- wahandisi, Daktari, Prof, wachumi, wahasibu, wataalam Rasilimali watu, marubani nk.
Ndugu wananchi wa Wilaya ya Morogoro, shimeshime kwa heshima kubwa na taadhima naomba kama kawaida yetu tujitokeze kwa wingi kuulaki Mwenge wetu wa Uhuru.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA, NAWATAKIA MAANDALIZI MEMA YA KUUPOKEA MWENGE WA UHURU.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa