MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, amezindua rasmi Mashindano ya Bonanza la Morogoro Oktoba Tunatiki 2025.
Mashindano hayo yamezinduliwa Julai 22-2025 katika uwanja wa Shujaa Manispaa ya Morogoro.
Mashindano hayo yaliyoanzishwa na DC Kilakala, yameshirikisha timu 4 ikiwemo timu ya Black Viba, Black People, Mawenzi na Damu Chafu FC.
Katika uzinduzi huo, Timu ya Black Viba yenye maskani yake Vibandani Kata ya Mbuyuni Manispaa ya Morogoro imefanikiwa kutinga hatua ya Fainali baada ya kuinyuka Timu ya Black People bao 1- 0 katika mchezo wa utangulizi wa mashindano ya Bonanza la Morogoro Oktoba Tunatiki 2025.
Akizungumza na Wananchi, DC Kilakala, amesema lengo la Bonanza hilo ni kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi juu ya kushiriki kikamilifu katika kupiga kura kwenye uchaguzi Mkuu wa kuwachagua Viongozi mbalimbali ikiwemo Madiwani, Wabunge na Rais Oktoba 2025.
Aidha, DC Kilakala, amewataka wachezaji kutumia Bonanza hilo kuzalisha vipaji, kudumisha amani na kutengeneza fursa ya ajira kupitia Bonanza hilo la kimichezo ili Morogoro iendelee kuzalisha wachezaji wengi maarufu kama Dickso Job, Kibwana Shomary n.k.
Pia , DC Kilakala, amesema mshindi wa kwanza wa Bonanza hilo atazawadiwa Milioni 5 mshindi wa pili milioni 2, mshindi wa tatu milioni 1 na mshindi wa nne shilingi laki 5 huku zawadi za wachezaji Bora na marefa zitatolewa pia.
Mchezo wa nusu fainali ya pili utafanyika Julai 25-2025 utakutanisha timu ya Mawenzi na Damu Chafu FC kwenye uwanja wa Shujaa na fainali itachezwa Julai 31-2025 ikitanguliwa na mchezo wakutafuta mshindi wa tatu.
Mwisho, DC Kilakala, amesema mara baada ya kumalizika kwa fainali , kutakuwa na burudani kalii kutoka Kwa wasanii mbalimbali kutoka Zanzibar na Tanzania bara watakaotoa burudani hadi mishale ya saa 6 usiku ili kuwapa raha Wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa