MHAKIKI wa Mashindano ya afya na usafi wa Mazingira Kitaifa kwa mwaka 2025 , Salvata Silayo, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,Emmanuel Mkongo, kwa uwekezaji alioufanya kwenye sekta ya afya na usafi wa mazingira hususani kwenye ujenzi wa Machinjio mpya ya kisasa Mkundi ,uboreshaji wa usafi Soko Kuu la Chifu Kingalu, miundombinu ya bora ya vyoo, mafanikio makubwa ya usajili wa majengo ya vyakula pamoja na uwezeshaji wa wataalamu wa afya na mazingira katika shughuli zao za kila siku.
Kauli hiyo ameitoa katika kikao cha majumuisho kilichowakutanisha wataalamu mbalimbali wa Idara na vitengo ikiwemo Mkuu wa Divisheni ya Afya ,Lishe na Ustawi wa Jamii, Mkuu wa Rasilimali watu na Utawala, Afisa Afya Manispaa, Afisa Mazingira, Afisa Udhibiti taka na usafishaji , Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro kilichofanyika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Emmanuel Mkongo, mara baada ya kupokea maelekezo ya maboresho ya usafi na afya kutoka kwa Mhakiki wa Usafi na Afya Kitaifa, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote ili kuhakikisha Manispaa ya Morogoro inaingia kwenye nafasi ya 3 bora ya usafi Kitaifa kutokana na uwekezaji ambao Manispaa imefanya hususani katika miundombinu ya unawaji wa mikono na udhibiti wa taka na usafishaji.
Aidha,Mkongo,amemuelekeza Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro kushirikiana na Afisa Afya wa Manispaa kuhakikisha wanaboresha maeneo yote ya miundombinu ya yanayohusisha masuala ya usafi wa vyoo.
Kwa upande wa Mratibu wa Mashindano ya Afya na Usafi Manispaa ya Morogoro, Ndimile Kilatu, ambaye pia ni Afisa Afya wa Manispaa ya Morogoro, amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro pamoja na Uongozi wa Manispaa kwa ushirikiano mkubwa wanaouonesha katika masuala mazima ya afya na usafi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa