Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya nne ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, amefungua rasmi maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na kupeana uzoefu na mawazo yatakayoleta mabadiliko katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mhe. Pinda amesema hayo Agosti 2, 2025, wakati akifungua maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) yanayofanyika katika viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere mkoani Morogoro, ambapo kaulimbiu ya maonesho hayo inasema, “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, 2025”.
Mhe. Mizengo Pinda amesema kuna umuhimu wa sekta binafsi na umma kuwa na ushirikiano wa karibu na kufanya kazi pamoja hususan katika nyanja za ufugaji, kilimo na uvuvi ili kuweza kuongeza thamani ya mnyororo wa mazao yatokanayo na sekta hizo kwa maslahi mapana ya taifa.
“Niwaombe sana wananchi: ushirikiano, ushirikiano miongoni mwetu; jambo la msingi sana,” amesema Mhe. Mizengo Pinda.
Aidha, Mhe. Pinda amesema ili kuwaletea maendeleo watanzania, lazima kuishirikisha Sekta binafsi kwa kuwapatia maeneo ya uwekezaji, Pia amewataka wananchi kuachana na jembe la mkono badala yake watumie zana bora za kilimo, mifugo na uvuvi zinazooendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Sambamba na hayo, Mhe. Mizengo Pinda amebainisha mazao yaliyoongoza kuingiza fedha kupitia mauzo ya nje hivyo kuchangia pato la Serikali kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025 kuwa ni pamoja na zao la ufuta limeingiza zaidi ya sh. trilioni 2.2, korosho sh.Bil. 931, tumbaku zaidi ya sh. Bil. 800, na mengine yaliyoongezwa thamani kupitia mfumo wa stakabali za ghala.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu huyo Mstaafu amewakumbusha wananchi kujitokeza na kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, kwani ni haki yao ya Msingi kumchagua viongozi wao ili waweze kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amemshukuru Mhe. Pinda kwa kukubali kushiriki ufunguzi wa maadhimisho hayo, pia amesema wataendelea kujipanga kuhakikisha maonesho yajayo yanakuwa mazuri kuliko yaliyopita.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki kwa mwaka huu wameandaa jukwaa la mafunzo ya mbinu bora za kilimo, mifugo na uvuvi, hivyo wananchi na wadau mbalimbali wameaswa kufika na kupata elimu ya sekta hizo ili ziweze kuleta tija zaidi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa