MKUU wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu Manispaa ya Morogoro ,CPA.Michael Mbembelwa, amewataka Wakuu wa Shule za Sekondari, Shule za Msingi na Vituo vya kutolea huduma za afya Manispaa ya Morogoro wakishirikiana na waweka hadhina wa Vituo vyao kuhakikisha wanatumia Mfumo wa EFFARS kikamilifu ili matumizi ya fedha zote zinazotakiwa kutumiwa ziwe zina idhinishwa na Mkurugenzi wa Manispaa
Hayo ameyasema Agosti 19-2025 ,akifungua Mafunzo hayo ya maboresho katika Mfumo wa Uhasibu na Utoaji wa Taarifa za kifedha katika Vituo vya kutolea huduma (Effars) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Stendi ya Mabasi Msamvu.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, CPA. Mbembelwa, amesema mfumo huo wa EFFARS umetayarishwa ili kukidhi mahitaji ya stadi sahihi (zilizoboreshwa) za udhibiti wa fedha katika ngazi ya kituo vya kutolea huduma pamoja na kuondoa matumizi ya Hundi (Check).
CPA. Mbembelwa,amesema Mfumo huo wa EFFARS umejikita zaidi kuondoa matumizi ya hundi ambayo Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi za kulipia hundi ambapo mfumo huo utamruhusu mtu mmoja ambaye atakuwa anaruhusu malipo kufanyika Benki kwa njia ya mfumo na kumfikia mteja moja kwa moja.
Ameongeza kuwa EFFARS umejikita katika maeneo ya kuweka kipengele cha kibali cha matumizi (expenditure permit) ambacho kitamlazimu Mkurugenzi wa Manspaa kujua aina ya matumizi ambayo yanakwenda kutumika ili aweze kutoa idhini ya matumizi hayo na kibali hicho kinatoka moja kwa moja kwenye mfumo wa EFFARS.
Amesema baada hati ya malipo kukamilika,itapitiwa na mweka hadhina wa Manispaa kwa ajili ya kuifanyia ukaguzi kisha atairuhusu na kupitia mfumo wa malipo ya Serikali wa MUSE ambapo Mhasibu wa MUSE ataruhusu malipo kwenda Benki na kuendelea na taratibu za malipo.
Aidha,CPA.Mbembelwa, amesema mfumo wa EFFARS umelenga zaidi katika kufanikisha malipo kufanyika kwa haraka zaidi ukiliganisha na sasa, ulinzi na usalama wa taarifa za malipo ya wateja,uzingatiaji wa sera,, sheria , kanuni na usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali.
Mafunzo hayo yanaendelea Agosti 20-2025 yakishirikisha Wahasibu wa Vituo vya kutolea huduma za afya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa