MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amekutana na Wamiliki pamoja na Meneja wa Hoteli Wilayani Morogoro kwa ajili ya kuwapatia elimu pamoja na maelekezo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli, juu ya kuwapokea raia wa kigeni katika Hoteli zao ikiwa na lengo la kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Mkutano huo umefanyika leo Aprili 3, 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Wamiliki hao na Mameneja wa Hoteli , amesema lengo la mkutano huo ni kuwapa maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli juu ya kuwapokea raia wa kigeni katika Hoteli zao ikiwa na lengo la kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Amesema kumekuwa na utaratibu wa kuwakumbatia watu wasio julikana katika nyumba za kulala Wageni hususani katika Hoteli jambo ambalo ni baya sana hasa katika kipindi hiki cha kupambana na vita dhidi ya Ugonjwa wa CORONA.
Chonjo, amesema ni wakati wa kushirikiana na kuwa kitu kimoja kati ya Serikali na Wamiliki wa Hoteli kwa ajili ya kuwachunga na kuwatolea maelezo raia na washukiwa wanaoingia katika Hoteli zao kwa kuwawekea ulinzi endapo watawabaini ili kutoeneza ugonjwa huo.
“Tumeitana hapa kwa lengo moja, Mhe. Rais Dkt John Magufuli ameshatoa maelekezo kwa Hoteli zote jinsi ya kuweka umakini na wageni wanaotoka nchi zilizo na historia ya Ugonjwa huo, kwahiyo tunatakiwa tushirikiane kwa pamoja na tutoe ushirikiano wa kuweka mazingira kwa washukiwa hao, kama utaona mtu haeleweki toa taarifa au ameingia katika Hoteli yako ni raia wa kigeni muhifadhi katika chumba chenye huduma zote ndani kwa muda wa siku 14 na asitoke nje baada ya hapo piga simu kwa wataalamu wa afya watakuja kumuangalia kitaalamu na baada ya siku 14 kama zitaonekana dalili za Ugonjwa huo atachukuliwa na Wataalamu kufikishwa katika Karantini zetu tulizozitenga maeneo, hawa sio kwamba wana ugonjwa ila tahadhari ni muhimu na chumba chake hakikisheni muhudumu haingii ndani , wala ndugu pamoja na familia zao na huduma za chakula anatakiwa awekewe nje ya mlango na kumgongea ili kukifuata na upande wa nguo zao lazima zifuliwe kwa dawa na kuwekwa katika vikapu zikikauka zipelekwe mlangoni kama ilivyo huduma nyengine , lakini baada ya mtu huyo kumaliza karantini hapo Hotelini chumba chake kitatakiwa kufanyiwa Farmigation ya hali ya juu na huyo mtu atajaza fomu ya kuonyesha kwamba alikuwa Karantini na yupo tayari kuwepo uraiani” Amesema DC Chonjo.
Aidha, amewatahadharisha Wamiliki kuacha tama ya pesa badala yake wawe makini katika kutanguliza afya za wahudumu wao pamoja na za Wananchi kwa ujumla kwani wanaweza kuwa na tamaa ya kupokea fedha nyingi wakati huo wanaleta ugonjwa na kuhatarisha maisha ya watu wengine.
Pia amesema ni vyema kujenga ushirikiano mzuri baina ya Wamiliki wa Hoteli, Maafisa Uhamiaji pamoja na Wataalamu wa afya ili wanapombaini mtu haeleweki au ana dalili za ugonjwa huo wakatoa taarifa mapema sana ili hatua za kitaalamu ziweze kuchukuliwa.
Hata hivyo,amewataka Wamiliki wa Hoteli wote kuanzia tarehe 6, Aprili siku ya Jumatatu , kila mmiliki awe ametoa taarifa ya huduma za bei katika vyumba vya kulala kwa Hoteli nzima na kukabidhi timu ya Wataalamu watakao pita mitaani kukusanya taarifa hizo ili wale wanaotaka kwenda kupata huduma kama itatokea anawekwa mtu Karantini basi alipe kulingana na uwezo wake wa fedha katika upatikanaji wa huduma hizo ili isije kuleta shida kwa wamilki wa Hoteli baada ya kushindwa kulipa huduma .
Amesema kuwa baada ya ugoinjwa huo kuingia hapa nchini, Wilaya ya Morogoro iliunda Kamati za Karantini, hivyo ni jukumu sasa la Kamati hiyo kuanza kufuatilia bei za vyumba vyote kwa kila Hoteli ili kuweza kuona jinsi ya kuwasaidia Wageni wanaotaka Hoteli kwa bei tofauti tofauti kulingana na uwezo wake wa kifedha.
Katika kuhitimisha mkutano huo, amesema kama watu wote watamuomba Mwenyezi Mungu na kuzingatia maelekezo ya Wataalamu pamoja na Viongozi wa Ngazi za juu na kufuata maelekezo yote basi ugonjwa huo kwa Wilaya ya Morogoro hautafika .
Katika hatua nyengine, DC Chonjo, aliwataka Waganga wakuu wa Manispaa ya Morogoro pamoja na Morogoro Vijini kuwasilisha taarifa ya jinsi walivyochukua hatua za kupambana na Ugonjwa wa CORONA.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Morogoro Vijijini, Dr. Robert Manyenyere , amesema wao walitumia njia za kutoa elimu katika maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu , kutenga eneo la Karantini katika Kituo cha afya cha Ngerengere, kutenga eneo la Karantini katika Bwawa la Mwalimu Nyerere, pamoja na kuweka kituo cha Karantini katika Mradi wa Mwendokasi kwani eneo hilo limekuwa na wageni wanaoendelea na ujenzi huo.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr. Gosbert Kalunde, amesema Manispaa ya Morogoro imetoa elimu katika meneo yote yenye mkusanyiko ikiwamo Nyumba za wageni, mama ntilie ,Matangazo katika Vyombo vya Habari, vituo vya Bajaji, Bodaboda, Madukani, Stendi za Daladala pamoja na Stendi kubwa ya Mabasi yaendayo Mikoani ya Msamvu lengo likiwa kuwaelimisha wananchi jinsi ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Amesema tayari Manispaa ilishaanda timu ya Wataalamu wa Karantini na eneo ilishatenga lililopo katika Ujenzi wa Hospitali ya Manispaa iliyopo Kata ya Mkundi ambapo washukiwa wote wa Ugoinjwa wa CORONA wanapekwa huko kwa jili ya vipimo vya awali.
Pia amesema wamenunua vifaa tiba kwa kuwakabidhi wauguzi waliopo katika Vituo vya afya pamoja na wale waliopo katika Karantini hiyo kuvitumia endapo watapata mshukiwa wa ugonjwa huo.
Licha ya jitihada hizo, lakini amesema wapo viongozi wa Manispaa kwa fedha zao wenyewe waliamua kuiunga Mkono Serikali kwa kugawa ndoo za maji , sabuni pamoja na vitakasa mikono kwa jili ya kuwakinga wananchi wao na ugonjwa huo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema baada ya agizo la Waziri Mkuu, Mh Kassim Majaliwa la kuwataka wafanyabiashara kuuza vifaa tiba kwa bei elekezi, yeye pamoja na timu yake ya Wataalamu walitembelea maduka hayo na kupiga faini baadhi ya maduka kwa kukiuka agizo la Waziri na kutoza faini kwa upande wa magari ambayo yalikiuka pia maagizo ya kuwawekea maji sabuni na vitakasa mikono abaria wao.
Paul Haule ambaye ni Mmiliki wa Bambo Guest House, amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa maelekezo aliyoyatoa na kuahidi kumpa ushirikiano katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa CORONA.
“Tunampongeza Mkuu wa Wilaya hakika kikao hiki ni chakujenga kwa pamoja, ugonjwa huu unaua ndugu zetu wanateketea katika Mataifa mengine , kwahiyo tukuhakikishie Mkuu wetu wa Wilaya maagizo kwa pamoja tumeyapokea na tunakwenda kuyafanyia kazi , wote tukishirikiana kwa pamoja ugonjwa huu utakuwa ni historia kwetu wananchi wa Morogoro” Amesema Haule.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa