Mkuu wa Wilaya ya Morogoro mheshimiwa Rebbeca Nsemwa, amewataka vijana kuwa wazalendo kwa kufanya mambo yenye faida kwa nchi, na yanayotetea maslahi ya nchi huku wakiepuka kutumia maendeleo ya kiteknolojia kupotosha maadili ya kitanzania.
Nsemwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na vijana wanaotarajiwa kushiriki kwenye mdahalo utakao fanyika kwenye usiku wa mkesha wa Mwenge wa Uhuru Jumamosi, tarehe 27.04.2024 katika uwanja wa shule ya msingi K-Ndege Manispaa ya Morogoro.
Amewataka vijana kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri, kwa kuwa mikopo hiyo itawasaidia kujikwamua kiuchumi na kupambana na changamoto ya ajira, inayowakabili vijana wengi hivi sasa.
Katika hatua nyingine mheshimiwa Nsemwa ameitaka jamii kuwa karibu na vijana, na kuwapa malezi bora ili kuwalinda na mambo yanayoweza kuleta madhara makubwa kwa Taifa na nguvu kazi yake kwa ujumla, ikiwemo suala la mahusiano ama ndoa za jinisia moja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Morogoro ndugu Emmanuel Mkongo, amewataka vijana kuwa na mtazamo chanya kuhusu Mwenge wa Uhuru, na kuhakikisha wanachangamkia fursa zinazopatikana ndani ya mkoa wa Morogoro hasa katika sekta za kilimo na uvuvi.
“Msiutazame Mwenge wa Uhuru kama utambi unaowaka na kutoa moshi, bali tambueni kwamba wenyewe ni tunu ya Taifa letu, inayohamasisha masuala ya uzalendo, upendo, amani na utulivu.
“Kila mara Mwenge wa Uhuru unapopita kwenye maeneo yote nchini huwa unasisitiza dhima ya Taifa, ya kupambana na rushwa na dawa za kulevya, ambazo hivi karibuni zimekuwa zikichangia sana kuathiri afya ya akili ya vijana wanaozitumia” alieleza Mkongo.
Aidha, Mkongo amewataka vijana kutumia mdahalo huo kupata mawazo chanya na maarifa mapya, yatakayo wajenga, kupata stadi za maisha na kujadili nchi yetu ilikotoka na inakokwenda, kwa sababu wao vijana wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha nchi inasonga mbele.
Naye msimamizi mkuu wa mdahalo huo, Dkt. Massimba amewaasa vijana kuacha kualalamika mitaani, badala yake wazingatie uzalendo na wajue stadi za maisha za sasa ili waweze kutimiza ndoto zao.
Dkt. Massimba ametaja uadilifu, uaminifu, ukengeufu dhidi ya tamaduni na imani zetu, uongozi, uzalendo,rushwa, dawa za kulevya, na stadi za maisha kuwa ndizo mada zitakazo jadiliwa kwenye mdahalo huo wa usiku wa tarehe 27.04.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa