Mapema mwanzoni wa juma hili, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, mheshimiwa Adam Malima pamoja na sekretarieti yake walifanya kikao cha kwanza cha mapitio ya mpango na bajeti ya Halmashauri ya Manispaa Morogoro kwa kipindi cha miaka mitatu ya fedha, tangu 2020/2021 hadi 2023/2024, na mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kikao hicho kilichofanyika kwa siku mbili kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kuhudhuriwa na wataalamu wa Manispaa (CMT) pamoja na mkurugenzi wake, lengo lake lilikuwa ni kutathmini uhai wa Halmashauri kupitia utekelezaji wa shughuli zake za maendeleo, ili kuhakikisha Manispaa inakuwa na mipango yenye ufanisi, na inayojibu changamoto za wananchi.
Katika kikao hicho, menejimenti ya Manispaa ya Morogoro iliwasilisha mapato na matumizi yake, fedha zilizopelekwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo, vijana wanawake na watu wenye ulemavu, taulo za kike, chanjo, na chakula shuleni, kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2020/2021 hadi 2023/2024.
Pia menejimenti hiyo iliwasilisha mpango wa bajeti ya Manispaa wa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kisha Mkuu wa Mkoa, mheshimiwa Adam Malima akasema ujenzi wa milimani na mafuriko ni miongoni mwa mambo yanayohafifisha jitiada za Manispaa kuwa Jiji hivyo mambo hayo yanapaswa kushughulikiwa kwa weledi na ufanisi hatimaye Manispaa iweze kukidhi vigezo na kuwa jiji.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa akaiagiza Manispaa kuwekeza zaidi kwenye maeneo ya milimani kwa kupanda mazao ya kimakakati kama vile karafuu, ili baada ya miaka mitano Halmashauri iweze kuanza kunufaika na uwekezaji huo.
“Cha msingi hapa tusijaribu, tuwekeze kikweli kweli kwa ‘target’ ili baada ya miaka mitano huko mbele basi tuwe tunapata kitu kinachotambulika” alieleza Dtk Mussa.
Kikao cha tathmini ya hali za Halmashauri kimefanyika kwa Halmashauri zote tisa za mkoa wa Morogoro tangu tarehe 31.01.2023 hadi tarehe 05.02.2024.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa