Tarehe 28.04. 2024 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro mheshimiwa Rebecca Nsemwa, alipokea kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mheshimiwa Dastan Kyoba, Mwenge wa Uhuru pamoja na wakimbizaji wake wa kimkoa na kitaifa.
Mara baada ya kuuopokea Mwenge wa Uhuru, mheshimiwa Nsemwa alitoa salamu za ukaribisho ambapo alieleza kwamba katika Wilaya ya Morogoro, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 216 ukitembelea miradi 18 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 6.6.
Mheshimiwa Nsemwa pia amemshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuiletea Wilaya ya Morogoro fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo kwa kweli imesogeza huduma bora kwa wananchi wa Morogoro.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa (2024) ndugu Godfrey Eliakim Mnzava, amesema agenda kuu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni kuhusu utunzaji wa mazingira na uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mnzava amesema Mwenge wa Uhuru unawaagiza wale wote wanaotaka kuwania uongozi wa Serikali za Mitaa kama wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji, wajumbe wa kamati za mitaa na wa Halmashauri Kuu za vijiji na vitongoji wachukue fomu kwenye vyama vyao vya siasa na fomu ya Serikali ili kupata ridhaa ya kugombea.
Kwa upande wa wananchi, Mnzava amesema Mwenge wa Uhuru unasisitiza kwamba ifikapo wakati wa kampeni wananchi wajitokeze kufika kwenye viwanja vya kampeni ili kuhakikisha wanasikia sera, mipango, maono na mawazo ya wagombea ili wakati wa kuchagua wachague viongozi kutokana na sera na mipango ya viongozi hao.
Vilevile, Mnzava amewataka wananchi wadumishe amani, utlivu na usalama katika maeneo yao wakati wa kipindi chote cha uchaguzi.
Kuhusu utunzaji wa mazingira, Mnzava amesema uchafuzi na uharibifu wa mazingira unaotokana na watu kukata miti hovyo, kuchoma misitu na mapori, shughuli za kilimo zisizozingatia uendelevu na uhifadhi wa mazingira, uchimbaji wa madini, ufugaji wa mifugo mingi bila kuzingatia nyanda za mailisho, na shughuli za viwanda zisizo zingatia uhifadhi wa mazingira, ndio sababu za kuwepo kwa ukame, joto, ardhi kupoteza rutuba, mafuriko na maporomoko.
Mnzava amewataka viongozi na wananchi kushirikiana kwa nguvu kabisa kuhakikisha kwamba wanaendelea kuhifadhi mazingira kwa kuendelea kupanda miti, kuhifadhi na kutunza mazingira ili mazingira nayo yawatunze.
Aidha, Mnzava amepongeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Morogoro kwa kufanya manunuzi yote kupitia mfumo wa NeST kisha akaagiza Taasisi zote za Serikali zihakikishe manunuzi yote ya umma yanafanyika kupitia mfumo huo ili kudhibiti ubadhilifu wa fedha za Serikali.
Miongoni mwa miradi iliyotembelwa na Mwenge wa Uhuru katika Manispaa ya Morogoro ni mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kauzeni kwenye kata ya Kauzeni, mradi wa miti wa Mindu kata ya Mindu, ujenzi wa barabara ya kiwango cha zege, ya Kichangani kata Kichangani, ujenzi wa shule ya msingi Viwandani kata Mafisa na ujenzi wa jengo la utawala shule ya sekondari Mkundi kata Mkundi.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa