WASIMAMIZI wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata Jimbo la Morogoro Mjini wameanza rasmi mafunzo Agosti 4, 2025 katika Ukumbi wa Mbaraka Mwishehe, huku wakila kiapo Cha kutunza Siri pamoja na tamko la kujitoa katika chama Cha Siasa.
Akitoa maelekezo baada ya zoezi la kiapo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Morogoro Mjini, Elizabeth Ngobei, amewataka wasimamizi hao wa Tume kufanya kazi kwa kuzingatia viapo vyao huku akionya swala la kufanya kazi kwa mazoea badala yake kujikita kusoma na kuelewa miongozo iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
"Mafunzo haya ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29-2025,someni kwa umakini Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume na ulizeni ili mpate kufafanuliwa kwenye maeneo ambayo kwa namna moja au nyingine pengine yatakuwa na changamoto za kufahamu ili kuwarahisishia katika utekelezaji wenu wa kazi za uchaguzi." Amesisitiza Ngobei.
Hata hivyo,amesema mafunzo hayo yameshirikisha wasimamizi wasaidizi 58 wa Uchaguzi kutoka Kata 29 ambapo jumla ya mada 11 zimeweza kuwasilishwa.
Pia,amesisitiza ushirikiano wa kujengeana uzoefu kutokana na baadhi ya wasimamizi wengine kuwa wapya na wengine kuwa na uzoefu wa usimamizi huo.
Aidha, Ngobei, amewataka wasimamizi hao wa Uchaguzi ngazi ya Kata kuzingatia viapo hivyo ili kuepuka uwajibishwaji utaotokana na ukiukwaji wa viapo hivyo.
Mafunzo hayo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata yanatarajiwa kutamatika Agosti 6- 2025
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa