Watoa huduma za afya ngazi ya kituo, wa Manispaa ya Morogoro wamezungumza na wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili, wa shule ya sekondari Kola Hill kuhusu elimu ya uzazi na huduma rafiki kwa vijana, ukatili wa kijinsia, makuzi ya vijana wakati wa umri wa balehe, mimba za utotoni, magonjwa ya kuambukiza yatokanayo na zinaa, na masuala ya lishe.
Herieth Lupembe, ambaye ni mtoa huduma za afya aliyetoa mada katika mzungumzo hayo yaliyofanyika tarehe 26.03.2024 shuleni Kola Hill amesema, lengo la mazungumzo hayo ni kuwafanya vijana wajitambue, na watambue nafasi zao katika jamii ili waweze kutimiza ndoto zao.
Katika mazungumzo hayo, vijana wametakiwa kuwa wawazi na kutoa taarifa kwenye sehemu husika pindi wanapopata changamoto za ukatili wa kijinsia, sambamba na kuwaelimisha na kuwasaidia ndugu zao kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia .
Pia wameambiwa kuhusu mabadiliko ya kimwili na kitabia wakati wa balehe na wametakiwa kutambua afya ya uzazi salama ili waweze kuepuka mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikichangia kukatisha ndoto za watoto wengi wa kike.
Aidha, wanafunzi hao wameaswa kuzingatia masuala ya lishe kwa kuhakikisha wanakula vyakula kutoka kwenye makundi yote sita ya vyakula ili waweze kuwa na afya njema kimwili na kiakili.
Mazungumzo haya yanayoendeshwa na watoa huduma za afya ngazi za vituo, wa Manispaa ya Morogoro yalianza tarehe 25.03.2024 na yanatazamiwa kufikishwa kwenye shule za sekondari, vyuo na kata mpaka tarehe 28.03.2024 yatakapo hitimishwa.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa