Leo, tarehe 30.11.2023, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, mheshimiwa Joyce Ndalichako amehitimisha shughuli za ‘kijiji cha vijana’ kwa kuwaasa vijana na hasa wa jinsi ya kike kufanya kila wawezalo kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU kwani takwimu za hivi karibuni zinaonesha kwamba, vijana wengi hasa wa jinsi ya kike ndio wenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU hapa nchini.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Morogoro, Waziri Ndalichako amewataka vijana kutumia elimu waliyoipata ndani ya wiki hii katika ‘kijiji cha vijana’ kuboresha shughuli zao na kujilinda dhidi ya matendo yanayoweza kuhatarisha afya zao na maisha yao.
“Takwimu zinaonesha vijana wengi hawatambui hali zao za kiafya, na hii inaweza kuchangia kuendelea kuongezeka kwa maambukizi mapya ya VVU, hivyo nitoe wito kwenu vijana mjitokeze kutambua hali zenu za kiafya ili kwa wale watakaogundulika kuwa na maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI, waweze kupatiwa huduma sawa na wanazopatiwa wale ambao tayari wanaishi na virusi hivyo.
Vilevile, mheshimiwa Ndalichako ametoa rai kwa wana habari kuendelea kutoa elimu kwa vijana hasa wasanii wa muziki wa Bongo Fleva kutumia fursa ya wao kupendwa sana na vijana walio wengi katika kuwafikishia jumbe mbalimbali kuhusu masuala ya UKIMWI na jumbe zitakazowasaidia kulinda afya zao.
Amewataka vijana wajue kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inawatambua, inawajali na kwamba itaendelea kuwaunga mkono ili kuhakikisha wanatimiza ndoto zao na kujikwamua kiuchumi kwa kuendelea kuibua miradi inayowalenga, ikiwa ni pamoja na mradi mkubwa uneondelea hivi sasa nchini, wa mafunzo ya kilimo kwa vijana, maarufu kama mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Vijana Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Nchini, Bi. Pudensiana Mbwiliza, ameishurkuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kutoa huduma bora za VVU na UKIMWI, hasa huduma ya utoaji bure wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARV’s), kwani kupitia huduma hiyo afya za vijana wanaoishi na VVU zimeimarika sana na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya ubaguzi na unyanyapaa unaotokana na kuwa na VVU.
“Kwa mujibu wa takwimu za UNAIDS, Tanzania ni nchi ya tano duniani kwa maambukizi mapya ya VVU na kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 ndilo linalotajwa kuwa kundi linalochagiza maambukizi mapya kwa kasi ya asilimia 30 kwa mwaka na kwamba kwa wastani kila wiki vijana 152 hupata maambukizi mapya, na kwa siku wastani wa vijana 22 hupata maambukizi huku sababu zinazotajwa kuchangia maambukizi hayo ni pamoja na kufanya ngono bila kutumia kondomu kwa usahihi, umaskini wa kipato, tamaa, mapenzi kati yao na watu waliowazidi umri na kutokufikiwa vyema na huduma za masuala ya VVU na UKIMWI” alieleza Bi. Mbwiliza.
Hatahivyo, Bi. Mbwiliza amesema vijana wanaoishi na Virusi vya UKIMWI hapa nchini, wanaishukuru Serikali kwa kuwashirikisha katika afua mbalimbali za masuala ya VVU na UKIMWI ikiwemo uundaji wa sera zinazohusu VVU na UKIMWI, kuwapatia mafunzo ya kuwajengea uwezo ikiwemo mafunzo ya masuala ya ufundi na stadi za maisha na kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, wamepatiwa mitaji kwa ajili ya kuanzisha shughuli zitakaziowawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Ndoto yetu sisi vijana tunaoishi na Virusi vya UKIMWI sio kuishi kwa matumaini au kama wagonjwa bali sisi ni vijana wenye afya, tunaojiamini, wajasiriamali, tunaoshiriki katika kulijenga Taifa letu kupitia juhudi zetu, maarifa na rasilimali tutakazowezeshwa na Serikali na wadau hatimaye tutoe mchango wetu kwenye maendeleo ya Taifa letu” alifafanua Bi. Mbwiliza.
Aidha, Bi. Mbwiliza ameiomba Serikali kupitia Ofisi za Maendeleo ya Jamii zilizopo kwenye Halmashauri zake iweze kuandaa utaratibu wa kufufua Klabu za vijana wanaoishi na VVU, kuendeleza Klabu zilizopo na kuanzisha Klabu hizo katika maeneo ambapo hazipo, sambamba na kuzijengea uwezo Klabu hizo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa usimamizi na ushirkishwaji wa konga za vijana zilizo ndani ya Halmashauri hizo.
Maadhimisho ya Kilele cha ‘Kijiji cha Vijana’ ni miongoni mwa matukio ya kuelekea katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, maadhimisho yanayofanyika kila tarehe 01 ya mwezi Disemba kwa lengo la kuwakumbuka watu waliopoteza uhai wao kutokana na janga la UKIMWI, na kama Taifa siku hii hutumika kufanya tathmini ya mwendo ambao Taifa limekwisha kuupiga katika kupambana na janga la UKIMWI.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa